Jumanne 20 Januari 2026 - 18:30
Hawza ijiandae kwa ujasiri, elimu na hekima kwa ajili ya nyakati ngumu zijazo

Hawza/ Mkurugenzi wa Hawza za Kielimu nchini Iran, huku akibainisha sifa za Hawza ya kimapinduzi, alisema: Hawza ya kimapinduzi ni ile inayojitayarisha kwa ujasiri, kwa elimu, kwa hekima na bila woga kwa ajili ya mustakabali mgumu na wenye changamoto; na jukumu hili ni la makundi ya wasomi na waanzilishi wa mbele.

Kwa mujibu wa ripoti ya mwandishi wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Alireza A‘rafi, Mkurugenzi wa Hawza za Kielimu za nchi Iran, katika kikao cha mashauriano ya pamoja kati ya walimu na wanafunzi wa Hawza wanaohusika katika vikundi vya kutatua matatizo na vipaji bora, kilichoandaliwa na Naibu wa Elimu wa Hawza za Kielimu mjini Qum Iran, baada ya kuwapongeza, alisema: Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu aendelee kuipa heshima bendera, mfumo, Mapinduzi ya Kiislamu, na afya njema pamoja na ustawi unaozidi siku hadi siku wa Kiongozi Mkuu, na kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, sisi sote tuwe askari wa Uislamu na Mapinduzi ya Kiislamu.

Mkurugenzi wa Hawza za Kielimu aliendelea kusema: Uongozi wa Hawza unaamini kikamilifu yote yaliyobainishwa na Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi kuhusu “Hawza yenye uongozi na umahiri wa juu”. Kile kilichobainishwa kina pande mbili: upande mmoja ni Hawza iliyofanikiwa ya sasa yenye orodha ndefu ya mafanikio, ambapo kazi nyingi zimefanyika; na upande mwingine ni Hawza ambayo imebaki nyuma ya msafara na inahitaji juhudi zaidi. Sababu ya kubaki nyuma ni kwamba dunia na Iran zimebadilika.

Ayatullah A‘rafi alisisitiza: Ni lazima tuutazame ukweli kama ulivyo na tuupange; hakuna jambo linalopaswa kuzuia kutambua mapungufu na kufanya juhudi za kuyatibu, na ikiwezekana, kuchukua hatua za kuyazuia mapema madhara yanayotarajiwa.

Mkurugenzi wa Hawza za Kielimu, akirejea hali maalumu ya wanazuoni wa kidini, alisema: Hali ya wanazuoni na taasisi ya dini kwa wakati mmoja ni ya uongozi na yenye athari kubwa, lakini pia ni nyepesi kuvunjika na inakabiliwa na mashambulizi yasiyo na kikomo. Kwa kuzingatia hali, hasa katika miaka miwili iliyopita, huenda tukasema kwamba kwa karne nyingi hali kama hizi hazijawahi kuwepo.

Ayatullah A‘rafi, katika kufafanua maana ya Hawza ya kimapinduzi, alisema: Hawza ya kimapinduzi ni ile inayojitayarisha kwa ujasiri, kielimu, kwa hekima na bila hofu kwa ajili ya nyakati ngumu na changamoto zilizo mbele yake; na hili ni jukumu la makundi ya wasomi na waliotangulia mbele.

Mkurugenzi wa Hawza za Kielimu aliongeza kuwa: Uongozi wa Hawza, katika kukabiliana na mkusanyiko wa masuala yaliyopo katika miaka hii, umepanga mipango yake kwa mujibu wa maelekezo ya Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi na Maraaji‘ wakubwa wa taqlidi, na imejitahidi kuchukua hatua za msingi na muhimu kwa kuzingatia maelekezo hayo.

Aliendelea kusema: Katika miaka ya mwanzo ya kazi yetu, nguvu nyingi ziliwekezwa katika kuandaa nyaraka za msingi kwa namna iliyojikita. Sambamba na kazi za kawaida, mfumo wa nyaraka za msingi na nyaraka elekezi za Hawza ziliandaliwa. Kwa kuzingatia nyaraka hizo, tuliandaa kwa majaribio mpango wa miaka mitano, ambao mwaka huu umefikia mwisho wake, na sasa tunaanza mpango wa pili wa miaka mitano. Ndani ya mipango hii, zaidi ya hatua 100 muhimu sana zimebuniwa, ambapo angalau hatua 50 ni kazi halisi, muhimu na za kimabadiliko.

Mjumbe wa Baraza Kuu la Hawza za Kielimu aliendelea: Miongoni mwa mitazamo hii, msingi mkuu umekuwa huu wa kwamba; asili na utambulisho wa Hawza — ambao ni muhimu sana — lazima ulindwe na uzingatiwe.

Ayatullah A‘rafi pia alisisitiza mtazamo wa kufunguka kwa Hawza kuielekea jamii (mtazamo wa nje), akisema: Umakini wa kielimu, mila thabiti za Hawza na kina chake vinapaswa kusonga sambamba na kulindwa. Wakati huohuo, mtazamo wa kuelekea nje, uzalishaji wa nadharia, nadharia za msingi, uzalishaji wa tafiti na kutatua matatizo pia vinapaswa kuwepo. Haya yanahusiana na masuala ya uongozi wa jamii na utawala, na mitazamo hii kadhaa lazima ikamilishane.

Mkurugenzi wa Hawza za Kielimu, akirejea hatua zenye athari zilizochukuliwa, alisema: Mojawapo ya kazi zenye thamani na umuhimu mkubwa zilizobuniwa na kuanzishwa katika Hawza ni "kamati za uongozi wa kimkakati", ambazo kupitia hizo, barabara kuu imefunguliwa ili Hawza iingie katikati ya mfumo wa utawala na iweze, kwa elimu na mantiki, kusimamia hoja zake kwa uthabiti. Sehemu nyingine ni mikataba ya ushirikiano, ambapo Kituo cha Mawasiliano kati ya Hawza na Mfumo wa Utawala kilianzishwa na kinafanya shughuli zake.

Aliendelea kuwa: Upanuzi wa masomo ya "dars al-kharij", upanuzi wa taaluma na mielekeo mbalimbali, usajili wa masomo huru, mpango wa kuelekeza mafao kuelekea majukumu ya msingi, mfumo wa watafiti na upangaji wa viwango vya watafiti, na mengineyo, ni miongoni mwa hatua muhimu zilizotekelezwa.

Ayatullah A‘rafi alihitimisha kwa kusema: Hatutaki tu matokeo ya mwisho ya kutatua matatizo; bali jukumu letu ni kulea rasilimali watu wenye uwezo na ufanisi. Watu hawa wanapaswa kutambuliwa darasani na kuungwa mkono ipasavyo.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha